Katika ulimwengu huu kuna usemi usemao ubinadamu ni kazi, hii ikiwa na maana ya kwamba ni bora uishi na wanayama pori kuliko kuishi na binadamu, binadamu anamaisha fulani ambayo hayawezi kukufurahisha kila wakati, wapo baadhi ya watu wao kazi ni kuwaaudhi wenzao. Hivyo ili uuweze kuishi maisha mazuri unatakiwa kujua kuishi na watu vizuri kama ifutavyo:
1. Epuka hasira za ovyo na kila mtu, kuwa msikivu kabla ya kukimbilia maamuzi (elewa kuwa ukiwa na hasira huwezi kupata suluhu ya jambo)
2. Usiwatendee wengine ubaya ukadhani kuwa utakuwa salama (ubaya hulipwa kwa ubaya, ipo siku ubaya wako kwa wengine utakurejea kama sio kuwarejea watu wa kizazi chako)
3. Usichukue maamuzi kabla ya kutafiti ukweli (pengine wapo wanadamu wanaopenda kuonekana wao wema kwa kuumiza wengine). Mtuhumu mtu lakini mpe muda wa kumsikiliza, usimshambulie mtu kwa maneno makali bila kuujua ukweli, ukijua ukweli nafsi inaweza kukusuta.
4. Mchukulie kila mwanadamu ni mkosaji (tambua kuwa hata wewe unawakosea sana wengine na wanakuvumilia. Hivyo usiwe mwepesi wa kuwaadhibu wenzio kwa ubaya).
5. Usipande mbegu ya chuki na ubaya katika jamii unayoishi ukadhani itakuacha salama (chuki hukua kama mti utambaao, ukiipanda ndani ya jamii yako, haitatoka kwako na inaweza kutafuna kizazi chako ukajutia.
6. Tambua kuwa yule unayeishi nae ni mwanadamu kama wewe, mpe heshima na mwonyeshee upendo hata kama huoni anafanana nawe. Maisha ni duara huenda ulikuwa kama yeye au atakuja kuwa kama wewe baadae.
6. Usiwe muongeaji ovyo ovyo na usiye na subira. Kuongea sana kunapoteza busara.
7. Jiepushe na maisha ya kusukumwa na wengine kufanya jambo usilojua manufaa yake. Jifunze kujitegemea kiakili. Sio kila unayemdhania rafiki moyoni mwake yupo pamoja nawe, na ukashirikiana nae, wengi wa marafiki zetu hututumia sana kuliko tunavyoweza kuwatumia wao.
8. Usipende sana kugombana na watu kwa njia ya maongezi yanayodumu kama vile, ujumbe wa maandishi, mawasiliano ya simu au ujumbe wa maneno (SMS). Kumbuka kuwa maneno yanaishi kuliko ugomvi au uadui, ipo siku yatakurudi na utajiona mpumbavu na kukosa pa kujificha. Jifunze kusubiri.
9.Usifumbue mdomo wako kutamka ubaya au kunyanyua kidole chako kuandika ubaya juu ya mwenzio bila kujiuliza mara mbili moyoni mwako hatima ya unachokitoa kwa mwingine.
10. Jishushe na jifunze kusikiliza wengine wakati wa mazungumzo ili uweze kujifunza kabla ya kukurupuka kujibu, usikivu ni kipimo cha busara, mtu anayekurupuka kujibu jibu kila anachosikia hawezi kuwa kiongozi, Mume au Mke mwema kwani mara nyingi atapotoka tu.
10. Usitunze hasira nyingi moyoni kwani hasira hukaa kifuani mwa mpumbavu. Jitahidi pia kuepuka kuwa na hasira mara kwa mara na zisizo na maana. Elewa kuwa hasira zisizo maana hukupunguzia maisha na kukupa maumivu wewe mwenyewe kuliko yule uliyemfanyia hasira, utakufa kwa magonjwa kabla ya wakati ufaao.
11. Thamani yako inategenezwa na watu wengine, wewe kama ni mtoto, mheshimu sana mzazi wako na kama umeoa au kuolewa, heshimu wazazi na familia ya mke au mumeo kwa kuwa bila wao, usingekuwa hivyo ulivyo leo unajivunia ndoa njema, kwa kuwa yupo mtu alimzaa huyo mwenzio. Mheshimu kwa lolote liwe jema au baya, utalipwa kwa wakati ufaao.
13. Usijibizane na mtu usiyemjua au ambaye hawezi kukupunguzia kitu katika maisha yako. Tambua kuwa unapunguza sehemu kubwa ya maisha yako kwa kutafuta magomvi na mtu wa mbali nawe.
14. Kumbuka asili yako, kumbuka upo hapo kwa kuwa kuna mahali ulitoka, maisha yanabadilika, usidharau pale ulipokuwa zamani kwa kuwa ndipo palipokufanya leo uwe hapo.
15. Subiri, sikiliza, elekeza, vumilia. Elewa sio kila mtu ana uelewa kama wako. Jitahidi kuwa mvumilivu katika kila jambo, usiinuke kuwafokea au kuwakaripia wengine kwa jambo ambalo pengine nao wanahitaji muda kueleweshwa ili walifanye vyema. Kumbuka sana, kuna wakati nawe ulikuwa huelewi kabisa lakini wapo wenzio walikuvumilia, wakakuelekeza njia njema, kufokea wengine mara kwa mara sio njia njema ya kuwafundisha bali ni kuwaweka mbali nawe.
0 Comments