Watu wasiofaa wapo kila mahali, kwa hakika wanakwaza na kurudisha maendeleo ya watu nyuma. Ukiwa kama mjasiriamali au mtu mwingine yeyote unatakiwa kufanya bidii kufikia malengo yako bila kuruhusu aina za watu wasiofaa kukuvuruga.
Inawezekana unawafahamu watu ambao ni sumu; yawezekana wanafanya kazi na wewe, ni marafiki zako au unaishi nao. Kadri unavyowaepuka katika maisha au kazi yako ndivyo mambo yatakavyozidi kuwa mazuri.
Fuatana nami katika makala hii nikushirikishe aina za watu ambazo ni sumu unazotakiwa kuziepuka katika maisha yako.
1. Watu wanaohoji kila kitu
Watu wanaohoji kila kitu hutafuta njia ya kupinga na kukosoa kila unachokifanya. Utatumia muda mwingi kuwaelewesha lakini watasikia kwa sikio moja na swala hilo kutokea sikio la pili. Kujaribu kutafuta msaada na ushauri kutoka kwa watu wa aina hii ni kupoteza muda.
Watu hawa huwa na maswali kama vile kwanini unafanya hivi? Unapoteza muda; si jambo zuri; la fulani liliharibika; nani kakuambia ufanye; nitapata nini mimi? hauwezi kufanikiwa kwenye hili labda tafuta jingine; linahitaji fedha nyingi mno n.k.
2. Wenye wivu
Safari ya mafanikio ina milima na mabonde, hivyo ni vyema kuwa na watu ambao watakuinua na kukutia moyo unapopita katika changamoto. Watu wenye wivu huamini kuwa kila kitu kizuri kinatakiwa kitokee kwao tu.
Watu hawa watafurahia unapopata matatizo tu, wala hawatakusaidia wakati wa changamoto. Hivyo ni vyema ukajiepusha na aina hii ya watu ili uweze kufanikiwa katika maisha yako.
3. Wajuaji
Wajuaji hawako tayari kuambiwa au kuelekezwa kitu chochote, kulingana na wao wanajua kila kitu na wanajua njia bora ya kufanya kila kitu. Si kwamba watu hawa hawahitajiki katika maisha ya mtu binafsi pekee, bali hata katika mazingira ya kazi.
Katika maisha upo usemi unaosema kuwa “wapishi wengi huharibu mchuzi”. Hivyo basi, kwa kuwa wajuaji hujifanya wanajua kila kitu na hawako tayari kupokea maelekezo, basi ni vyema ukawaepuka wasije wakakukwamisha.
4. Wenye kiburi
Watu wenye kiburi wamejaa katika jamii inayotuzunguka. Watu wenye kiburi hawaambiliki wala kushaurika, wao hufikiri ni bora kuliko kila mmoja anayewazunguka.
Unapofanya kazi na mtu mwenye kiburi ni vigumu kukaa naye pamoja mkapanga majukumu na yakatekelezwa; hivyo ni bora kuwaepuka.
5. Watu wenye visingizio na walalamikaji
Watu wa aina hii huwa hawaishiwi sababu, wao hulaumu kila kitu na kila mtu. Watu hawa hawakubali kupokea majukumu bali huwanyoshea wengine vidole; pia hawako tayari kuwajibika kutokana na makosa yao.
Mara nyingi watu hawa husingizia kitu au mtu mwingine kwa kila kosa wanalolifanya. Waondoe kwenye maisha, biashara au ofisi yako sasa ili uishi kwa amani na kuwa na mafanikio.
6. Wale wenye mawazo hasi au wapinzani
Mtu mwenye mawazo hasi atakausha nguvu zako za mawazo chanya. Watu hawa kila mara hujitahidi kukuvuta chini ili ufanane nao na kuamini kile wanachokiamini. Kamwe huwezi kupokea neno la hamasa kutoka kwao.
Watapuuza kila wazo jema ulilo nalo, watatafuta kila njia ya kukuonyesha jinsi utakavyoshindwa katika wazo lako kuliko utakavyofanikiwa. Hivyo ni vyema ukachukua hatua mapema ya kuwaepuka watu hawa.
7. Watu waongo
Ili kufanikiwa katika maisha unahitaji kuwa na watu ambao wanaaminika na kutegemewa. Unapokuwa na watu waongo ni vigumu kufanikiwa kwani utaamani mambo au taarifa fulani kumbe hazina ukweli wowote.
Hebu fikiri unafanya kazi na mhasibu mwongo; ataiba pesa au kupoteza taarifa kisha atakudanganya kuwa hajafanya hivyo; je unajua nini kitatokea? Utapata hasara; hivyo basi jitahidi kujiweka katikati ya watu wakweli.
8. Wambea
Aina hii ya watu ipo kila mahali, ofisini, nyumbani, shuleni n.k. Watu wambea hawawezi kutofautisha uzushi au uvumi na ukweli.
Watu wambea husambaza taarifa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine; kwa ufupi mtu anayekuambia taarifa za mwingine ndiye yeye huwaambia wengine taarifa zako. Wambea hutengeneza mazingira mabaya ya kazi yenye chuki na ugomvi. Hivyo ni vyema kuwaondoa watu hawa katika maisha, biashara au ofisini kwako.
Nakukumbusha usemi usemao “ukikaa na waridi pia utanukia”; hivyo ukikaa na watu wabaya pia watakuwa na athari mbaya katika maisha yako. Jitahidi kujiweka katika mazingira yenye watu wanaopenda kufanikwa na wenye mawazo chanya.
0 Comments