YA JUX NA VANNESA, PENZI LITAFANYA UCHEKWE

KUVUNJIKA kwa uhusiano wa kimapenzi kati ya mastaa wa Bongo Flava Vanessa Mdee na mtanashati wake Juma Jux kikweli kumeniumiza kwa asilimia fulani.

Sitadanganya, ipo wachumba wasanii ambao kila nikisikia wametengana wala huwa hata hainisumbui.

Kwa mfano Diamond kuachwa au kuachika, Timmy Tdat, Otile Brown na wengine wa sampuli hii.

Hawa ni wasanii ambao nimeshindwa kushawishika kabisa na staili yao ya mapenzi.

Sio kama ya Vanessa na Jux. Ya hawa huwa ni kama vile ya kuongopea.

Ni kama vile hao niliowataja huingia katika mahusiano kwa madhumuni ya kusaka faida fulani.

Ila inapofikia ya Vanessa na Jux, moyo wangu hunyong’onyea.

Hii naamini ni kwa sababu wasanii hawa wameweza kuthibitishia ulimwengu mapenzi ya kikweli.

Wanajua kupendana, hawaigizi, yaani kabisa unaona hisia zipo na ndio maana taarifa za wao kutengana takriban mwaka mmoja baada yao kurudiana, zimeniumiza utadhani na mimi nimehusika.

Vanessa amekuwa akionekana sana akila bata kule Ufaransa kwa mujibu wa posti zake huku dume lake likiwa linasotea nyumbani Dar es Salaam.

Ingelikua kama bado wapo vizuri, amini usiamini, wangeliambatana.

Kuna tetesi kwamba kuvunjika kwa uhusiano wao huenda kulichangiwa na madai ya mchepuko kwa upande wa Jux.

Sitaki kusadiki hilo kwa maana inaweza kuwa ni kweli lakini pia toka waliporudiana, wameonyesha mapenzi ya mia kwa mia.

Nataka kuamini kuwa ni tatizo ambalo linaweza kutatulika na wakarudiana.

Ila kama itatokea wakarudiana, basi ni muda sasa wajifunze kuyaweka mahusiano yao chini ya maji.

Mara ya kwanza walipotengana dunia nzima ilijua sababu waliishii kuitangazia dunia.

Ndio maana hata baada yao kutemana ilikuwa rahisi sana kwa mtu yeyote kubaini hilo.

Waliporudiana 2017, walizidisha dozi ya mapenzi kiasi cha wao kufanya shoo ya pamoja Tanzania nzima.

Mashabiki wang’amua

Sasa tena yamewakuta na ikawa rahisi mashabiki kung’amua kuwa mambo sio mazuri.

Awali zilionekana kuwa tetesi hadi alipothibitisha mdogo wake Vanessa, Mimi Mars kwamba uhusiano wao kwa sasa ni ule wa kishikaji.

Kilichonipasua kichwa hata zaidi ni kuyakumbuka maneno ya Mars akisema kuwa haamini ikiwa dadake ataishia kuolewa na Jux sababu wote hawajaonyesha nia ya kutaka kuwa na familia.

Hii kwangu mimi ikawa na maana kwamba wawili hawa japo wanafaana, wanapotezeana muda.

Inauma.

Ndio maana naamini kuwa kama mipango yao ni kudeti hadi siku ya kiama, basi wajitahidi kufanya siri endapo watarudiana ili hata watakapotemana mambo yatakuwa ya kimya kimya.

Hali hii wanayopitia mastaa hawa imenikumbushia mashairi ya wimbo wake Mondi Sikomi kwamba mapenzi ni safari unavyopita ndio jinsi unavyojongea ila tatizo hujui uendako.

Kwenye wimbo mwingine Mapenzi Basi Mondi aliinasa kabisa picha inayoendelea katika maisha ya Jux na Vanessa alipoimba kwa kusema haya mapenzi ndio basi tena sababu yamemfanya achekwe na kutukanwa.

Ndicho anachopitia Jux. Inauma ila ndio hali. Natumai wamejifunza kuwa kimya kina mshindo.

Post a Comment

0 Comments