JE, WAJUA NAMNA SAHIHI YA KUONDOA VINYWELEO KWENYE MWILI WAKO

Leo tutaangalia hatua za kufuata wakati wa kunyoa vinyweleo.

Uwepo wa vinyweleo vingi hasa katika maeneo ya mikononi na miguuni, hali ambayo huwakera watu wengi hasa wanawake ambao huona hicho ni kikwazo kikubwa cha kuonekana warembo.

Kutokana na wengi kujaribu kukabiliana na kero hiyo, wamejikuta wakitumia njia mbalimbali kuondoa hali hiyo hata wakati mwingine kuumia na kuiacha ngozi ya maeneo husika ikiwa imechunika au kuharibika na kusababisha madhara.

Wengi hupendelea kuviondoa vinyweleo hivyo kwa kuvinyoa, lakini mambo kadhaa yanatakiwa kufuatwa ili kufanikisha zoezi hilo na kuiacha ngozi ikiwa katika hali nzuri.

Jambo la kwanza, hakikisha unatumia mashine yenye wembe mpya, ili kurahisisha unyoaji kwani wembe butu utasababisha mnyoaji kutumia nguvu nyingi, hatimaye kuumiza na kujeruhi ngozi. Kabla hujaanza kuondoa vinyweleo, hakikisha unalowesha eneo husika, iwe ni miguu au mikono kwa muda usiopungua dakika mbili kwa kutumia maji ya baridi.

Unaweza kupaka krimu ya kunyolea au kulainisha ngozi, kisha anza kunyoa kwa kuipandisha mashine kutoka chini kwenda juu, ili kufanya vinyweleo vyote vitoke kwa urahisi na kuacha ngozi ikiwa laini bila makovu.

Tumia mkono kupapasa na kukagua kwa umakini eneo ulilonyoa, ili kujua kama umeondoa vinyweleo vyote. Ikiwa bado, rudia tena kunyoa hadi uhakikishe umevimaliza vyote.

Baada ya kumaliza, pakaa mafuta hasa ya maji ili kulainisha kabisa na kuondokana na mikwaruzo, ili kuvipa nafasi vitundu vya kupitisha hewa kwenye ngozi kufanya kazi yake.

Post a Comment

0 Comments