FAHAMU MAAMBUKIZI YA FANGASI SEHEMU ZA SIRI

Kati ya maambukizi yanayowasumbua wanawake wengi duniani ni maambukizi ya fangasi. Inakisiwa asilimia 75 ya wanawake wote duniani hupata maambukizi haya katika kipindi cha uhai wao.

Maambukizi ya fangasi katika sehemu za siri za mwanamke husababishwa na uwepo wa fangasi wanaojulikana kitaalamu kama Candida albicans.

Maambukizi haya pia hujulikana kama yeast infection au thrush. Fangasi hupatikana kama vimelea vya kawaida katika mdomo, mpira wa kupitisha chakula sehemu inayojulikana kama pharynx, katika kibofu cha mkojo, uume na hata kwenye uke.

Mfumo mzuri wa kinga wa mwili pamoja aina fulani za bakteria wanaoishi pamoja na fangasi hawa husaidia sana katika kuthibiti maambukizi yanayoyosababishwa na aina hi ya fangasi.

Nini hutokea?

Kwa kawaida, Candida albicans huishi kwenye uke na sehemu nyingine (kama zilivyoelezewa hapo juu) bila kusababisha madhara yoyote yale isipokuwa pale mazingira ya eneo husika yanapobadilika kama vile mabadiliko katika hali ya pH ya  eneo husika (ifahamike ya kwamba pH ya kawaida ndani ya  uke ni 4.0 - 4.5) au uwiano wake na vimelea  (microorganisms) wengine unapoharibiwa kutokana na sababu mbalimbali kama vile matumizi ya madawa aina ya antibiotics, kupungua kwa kinga mwilini kutokana na magonjwa mbalimbali n.k.

Maambukizi haya ya fangasi yanaweza kugawanywa katika sehemu kuu mbili

Maambukizi yasiyo makali yaani uncomplicated thrush: Katika kundi hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi  mara moja hadi nne kwa mwaka na dalili zake huwa si mbaya sana na maambukizi haya husababishwa na fangasi wa jamii hii ya Candida albicans.Maambukizi makali yaani complicated thrush: Katika kundi hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi zaidi ya mara nne kwa mwaka, dalili zake kuwa mbaya zaidi au kama maambukizi  yatakuwa yametokea kipindi cha ujauzito, ugonjwa wa kisukari, upungufu wa kinga mwilini. Aina hii kusababishwa na vimelea vya aina nyingine tofauti na Candida albicans.

Vihatarishi

Watu walio katika hatari ya kupata maambukizi ya fangasi hawa ni  wale wenye

• Kutumia sana dawa aina ya detergents kwenye sehemu za siri au douches (vifaa vinavyotumiwa kusafishia uke kwa kutumia maji yaliyochanganywa na siki au antiseptic yoyote ile) kwa sababu hali husababisha kuharibika kwa uwiano wa fangasi na aina nyingine ya vinyemelezi kama bakteria aina ya lactobacilli

• Kutumia sana madawa aina ya antibiotics, steroids ambayo yana tabia ya kushusha kinga ya mwili

• Mabadiliko ya mfumo wa homoni mwilini ambayo husababisha mabadiliko katika s ehemu za siri na hivyo kufanya kuwepo kwa ukuaji wa kasi wa fangasi hawa

• Ujauzito (kutokana na kubadilika kwa mfumo wa homoni mwilini na kupungua kwa kinga ya mwili). Hata hivyo ieleweke hapa kuwa si kila mjamzito hupatwa na maambukizi haya.

• Matumizi ya dawa za kupanga uzazi (vidonge vya majira)

• Upungufu wa kinga mwilini kutokana na magonjwa sugu kama kisukari, saratani aina yoyote ile, ugonjwa aina ya mononucleosis na nk.

• Ugonjwa wa ukimwi (HIV/AIDS)

• Matibabu ya homoni (hormonal replacement therapy) kutokana na sababu mbalimbali

• Matibabu ya kusaidia kushika mimba kwa wale wenye matatizo ya uzazi (infertility treatment)

• Msongo wa mawazo (stress)

• Utapia mlo (malnutrition)

• Kuvaa nguo au mavazi yanayoleta joto sana sehemu za siri kwa muda mrefu kama nguo za kuogelea (swimwear), nguo za ndani (chupi)  zilizotengenezwa kwa kitambaa aina ya nylon, nguo za ndani zinazobana sana nk.

• Kujamiana kwa njia ya kawaida mara tu baada ya kujamiana  kupitia njia ya haja kubwa (anal sex) au matumizi ya vilainishi venye glycerin wakati wa kujamiana pia yamehusishwa na maambukizi haya.

• Kuvimba kwa tezi la koo (goiter)

• Saratani ya tezi la koo (thyroid cancer)

• Wanawake wenye umri wa miaka kati ya ishirini na thelathini wapo kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi haya wakati wale ambao wameshaacha kupata hedhi au wale ambao hawajaanza kupata hedhi kabisa hawako kwenye hatari kubwa.

Kwa wanaume vihatarishi  vya maambukizi haya ni

• Kujamiana na mwanamke mwenye tatizo hili au maambukizi haya

• Upungufu wa kinga mwilini

• Matumizi ya madawa aina ya antibiotics kwa muda mrefu bila ushauri wa daktari

• Magonjwa sugu kama kisukari, saratani ya aina yoyote ile na nk.

Dalili na viashiria kwa wanawake

• Kuwashwa  sehemu za siri  (kwenye tupu ya mwanamke)

• Kuhisi kuwaka moto sehemu za siri (burning sensation)

• Kufanya kama vidonda katika sehemu za siri (soreness)

• Maumivu wakati wa kujamiana (superficial dyspareunia)

• Maumivu  au usumbufu wakati wa kujisaidia haja ndogo (wakati mtu anakojoa)

• Kuvimba na kuwa rangi nyekundu kwa  mdomo wa nje wa tupu ya mwanamke (labia minora)

• Kutokwa na uchafu wa rangi nyeupe au nyeupe kijivu, unaoweza kuwa mwepesi, majimaji au mzito na ambao umefanana na jibini (cottage cheese like discharge) wenye muonekano unaojulikana pia kama curd-like appearance. Kwa kawaida, uchafu huu haumbatani na harufu yoyote isipokuwa panapokuwa na tatizo la ziada kama ugonjwa wa zinaa aina ya Bacteria vaginosis. Uchafu huu unaotoka hapa unaweza kuenea kwenye maeneo mengine yaliyokaribu na tupu ya mwanamke kama kwenye mitoki (groin area) au perineum na kusababisha kuharibika kwa ngozi katika sehemu hizo.

Dalili na viashiria hivi huwa mbaya zaidi wakati  mwanamke anapokaribia  kupata hedhi.

Dalili na viashiria kwa wanaume ni

• Kuwashwa sehemu za siri

• Kuvimba na kuwa rangi nyekundu kwenye ncha ya uume

• Kuwepo kwa uchafu wa rangi nyeupe (kama nilivyoeleza hapo juu) kwenye sehemu ya juu ya uume.

• Kuwa na vidonda vidogo kwenye uume (sore on the glans)

Hata hivyo, mara nyingi wanaume hawaoneshi dalili zozote zile, ni vizuri kwa mwanamke kumueleza mwenza wake pale anapopata maambukizi haya ili naye pia apate kutibiwa.

Matibabu

Matibabu ya fangasi huusisha dawa za kutibu fangasi (antifungal drugs) kama vile dawa za kupaka za topical Clotrimazole, topical Nystatin, Fluconazole au topical Ketoconazole.

Wagonjwa wenye maambukizi yasiyo makali yaani uncomplicated vaginal candidiasis wanaweza kutumia dawa za kupaka (cream) kutoka dawa za fangasi za jamii ya -azole kama vile Butoconozale, Miconazole, Clotricomazole nk.

Dawa hizi hutumika kwa muda wa siku 3-7 kulingana na aina ya dawa. Mgonjwa anashauriwa kupaka dawa ndani ya uke pamoja na maeneo yote yanayozunguka sehemu hiyo. Jinsi ya kupaka dawa hizi ni kuanzia mbele kuelekea nyuma.

Aidha mgonjwa anaweza kupewa dawa za kutumbukiza ukeni ambayo atatumia kwa muda wa siku 3-14 kulingana na aina ya dawa. Dawa hizo ni pamoja na Miconazole, Tiaconazole, Terconazole, Nystatin nk.

Kidonge cha kumeza aina ya fluconzole pia huweza kutolewa. Dawa hizi nilizotaja hapa juu zina kawaida ya kuharibu ubora wa mipira ya kondomu zilizotengenezwa na mpira aina ya latex (latex condoms) pamoja na vifaa vya upangaji uzazi aina ya diaphragms.

Ni vizuri kwa daktari kabla ya kumpa mgonjwa dawa hizi kumfahamisha kwa ufasaha jinsi ya kuzitumia na tahadhari anayotakiwa mgonjwa kuchukua. Inashauriwa kama baada ya matumizi haya bado mgonjwa ana dalili za maambukizi au mgonjwa akapata tena maambukizi haya ndani ya miezi miwili baada ya matibabu ya awali, basi anashauriwa kwenda kumuona daktari ili apate matibabu zaidi.

Kinga ya maambukizi ya fangasi

• Kuosha sehemu ya siri kwa kutumia kitambaa kisafi kila siku na kuosha kuanzia mbele kuelekea nyuma, epuka kurudia ukishafika nyuma.

• Epuka matumizi ya sabuni zenye manukato, bubble baths, vaginal deodorant products, feminine hygiene, na bath powder.

• Vaa chupi ambazo hazibani sana na zilizotengenezwa kwa kutumia pamba au hariri (silk), epuka synthetic underwear.

• Epuka mavazi yoyote ya kubana kama jeans za kubana nk.

• Badilisha nguo za ndani (chupi) kila zinapopata unyevunyevu.

• Fua chupi zako kwa maji yenye nyuzi joto 90 na kuendelea.

• Tumia pad wakati tu unapozihitaji (kama umeingia kwenye mzunguko wako wa hedhi)

• Kula mlo wenye virutubisho vyote kamili (balanced diet)

• Epuka kufanya mapenzi  na mpenzi wako ambaye amepata maambukizi ya fangasi.

• Epuka kuoga  maji moto sana (hot baths) tumia maji ya uvuguvugu, hii kwa wale ambao wanaishi kwenye ukanda wa joto (tropical climate).

• Matumizi ya vifaa vya ngono (sex toys), vifaa vya upangaji uzazi (diaphragms, cervical caps) yanaweza kuleta kujirudia kwa maambukizi ya fangasi kama havitaoshwa  na kukaushwa vizuri baada ya kutumiwa.

• Baadhi ya tafiti zilizofanyika, zimethibitisha ya kwamba unywaji wa maziwa ya mtindi yenye live culture, husaidia kupunguza maambukizi ya fangasi.

Post a Comment

0 Comments