Mwanamitindo wa Kisomali raia wa Marekani amekuwa mwanamitindo wa kwanza Muislamu kuonyeshwa katika jarida la michezo Sports Illustrated akiwa amevaa burkini.
Halima Aden ameonyeshwa katika jarida la kila mwaka akiwa amevaa nguo hiyo ya kuogelea inayofunika mwili mzima isipokuwa uso viganja vya mikono na miguu.
"Wasichana wadogo wanaovaa hijab wanapaswa kuwa na wanawake wanaowatazamia katika kila sekta," ameiambia BBC.
Halima Aden alilelewa Kenya katika kambi ya wakimbizi , akahamia Marekani akiwa na umri wa miaka 7 na alianza kuvaa hijab muda mfupi baada ya hapo.
"Sasa tunawaona wanasiasa, wafanyabiashara wanawake, waandishi na watangazaji na wanawake wengine katika ufanisi wanaovaa hijab,na huo ndio ujumbe tunaohitaji kuutuma," amesema.
"Kumekuwa na muitikio mzuri na ni heshima kubwa kwangu kwamba Sports Illustrated limechukua fursa hii kuonyesha urembo walio nao wanawake wanaovaa kwa stara."
Sports Illustrated, lililowaonyesha nyota kama Tyra Banks na Beyonce katika ukurasa wake wa juu, ni jarida la Marekani linalosomwa zaidi na wanaume, na kumekuwa na hisia mchanganyiko kufuatia taarifa hii.
Mmoja aliandika katika Twitter: "Iwapo utaendelea kuvaa hijab na uufunike mwili wako- iwapo ukidhani ni sheria ya dini yetu au kwasababau unataka kuvaa mavazi ya stara - inakwenda kinyume kwa kupiga pozi linaloamsha hisia katika jarida linalofahamika kuwachukulia wanawaka kama vitu.."
Mwingine aliandika:"Ningeelewa iwapo ingelikuwa ni maonyesho ya kununua mavazi ya kuogolea kwa wanawake. Lakini kwa jarida lililonuiliwa wanaume, inakwenda kinyume kabisa na malengo ya hijab."
0 Comments