Sayari ya Mars imekuwa ikiwashangaza, kuwasisimua na kuwavutia binadamu kwa miaka mingi.
Maelfu ya miaka iliyopita, binadamu walikuwa wakishangaa na kujiuliza nini kinapatikana katika sayari hiyo inayopatikana umbali wa kilomita milioni 54.6 kutoka kwa dunia (maili milioni 34).
Sana, kutokana na muonekano wake wa rangi nyekundu sawa na ya chuma iliyoshika kutu, binadamu waliihusisha na moto au damu.
Jina Mars linatokana na mungu wa vita wa Warumi.
Kutokana na ufanisi wa kisayansi, binadamu kwa sasa amefanikiwa kufahamu mengi kuhusu sayari hii.
Sayari hii ina mandhari ya kushangaza: utayapata maeneo sawa na ya nyika duniani, maeneo ya jangwa kutokana na upepo mkali, mashimo makubwa yanayotokana na volkano, milima ya volkano na maeneo ya ukubwa sawa na taifa la Luxembourg yaliyojaa milima (machungu) ya mchanga.
Haya yote yamefunikwa na vumbi ya rangi moja
Ni eneo ambalo huwa hakuna mvua kamwe. Hakuwezekani kuwa na mvua kwani maji, iwapo yangekuwepo, hufusha na kuwa mvuke mara moja.
Katika sayari ya Mars, wakati sawa na wa kutua kwa jua duniani, anga hujaa rangi ya buluu. Dunia huonekana tu kama nukta tu miongoni mwa nyota angani.
Ni mandhari ya kupendeza sana hasa kwa wanaopenda utalii - ikizingatiwa kwamba binadamu hajatalii sana sayari hiyo, kuna uhakika kwamba iwapo utafanikiwa kufika huko, kila utatapoenda utakuwa binadamu wa kwanza kufika huko.
Utakuwa kama Wazungu waliokuwa wanatalii Afrika karne ya 19, ambapo walikuwa Wazungu wa kwanza kutazama milima, mito, nyika na misitu ya kupendeza barani. Lakini kumbuka kwamba hakuna oksijeni.
Utafikaje huko
Kwa karne nyingi, imekuwa ndoto tu lakini inakaribia kutimia. Iwapo mambo yote yatakwenda sawa, mjasiriamali mmiliki wa Space X Elon Musk anapanga kutuma kundi la kwanza la watalii kwenye sayari hiyo kufikia 2022.
Lakini gharama yake itakushangaza pengine. Tiketi ni $10bn! Lakini iwapo huwezi kupata pesa nyingi kiasi hiki, usife moyo. Kuna njia nyingine ya kiteknolojia ambayo taasisi ya safari za anga za juu ya Marekani Nasa inatafakari - kutumia miwani ya kisasa na roboti. Roboti ndiyo itakuwa Mars, wewe uwe papa hapa duniani lakini itakuwa ikikupeperushia picha za uhalisia kutoka sayari hiyo.
Vivutio sayari ya Mars
Kivuti kikuu ni mlima wa Olympus Mons. Mlima huu una urefu wa maili 14 (kilomita 22), na ndio mlima wa volcano mrefu zaidi katika Mfumo wa Jua. Kwa kulinganisha tu, urefu wa mlima huu ni mara tatu urefu wa mlima mrefu zaidi duniani, Mlima Everest.
Sawa na ilivyo kwa milima mirefu ya volkano duniani, mlima huu kilele chake kimefunikwa na mawingu - lakini si ya maji, bali ni ya vumbi.
Haijabainika iwapo mlima huu bado hulipuka, lakini inakadiriwa kwamba wakati mmoja ulilipuka na kurusha matope na mawe makubwa ya moto angani.
Ukisafiri kusini magharibi kutoka kwa mlima huu, utapata Valles Marineris.
Roboti hii ilipiga picha ya kwanza ya kujipiga (almaarufu selfie) katika Mars
Viumbe wote walio hai duniani huwa wana maji ndani yake. Hivyo, wataalam wamekuwa wakiamini kwamba iwapo kuna viumbe Mars, lazima wawe kwenye maeneo yaliyo na maji.
Kwa miongo mingi, wanasayansi walitafuta ishara za kuwepo maji Mars bila mafanikio.
Lakini mwaka 2011, walifanya ugunduzi huo. Waligundua michirizi ya maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka kwa milima na mabonde ya Mars. Inadhaniwa kwamba huenda mito, yenye maji yenye chumvi labda huchipuza kutoka chini ya 'ardhi' kwenye hazina kubwa ya maji.

0 Comments