Gari lolote zuri litaharibika kama halitunzwi vizuri. Vile vile, mipango mingi mizuri tuliyonayo na yenye kufaa katika maisha ni lazima itakuja kuanguka ikiwa itakosa umakini na udhibiti. Na ni matumaini yangu kwamba kila mmoja wetu hapa duniani ana ndoto, kila mmoja wetu anazo ndoto za maisha yake ya baadaye. Ndoto na malengo ya kuja kufanya mambo makubwa na kuwa mtu muhimu aliyefanikiwa. Ndoto hizi zinaonyesha lengo hasa la kupata kitu fulani. Lakini licha ya ndoto hizo na malengo kadha wa kadha tuliyonayo wengi wetu katika maisha. Ni wachache pekee ndio ambao wamekuwa wakiweza kufanikisha ndoto na malengo waliyojiwekea maishani mwao.
Na kuna sababu kadha wa kadha za kwa nini wengi hushindwa kufanikisha ndoto na malengo yao waliyojiwekea katika maisha. Wengi wetu tumekuwa na ndoto za maisha mazuri , tumekuwa na ndoto za maisha bora. Tumekuwa tukiweka malengo ila mwisho wa siku tunajikuta tukiwa palepale tulipoanzia, yaani hatusongi wala hatusogei. Ndugu rafiki elewa na utambue kwamba safari ya mafanikio katika maisha si lelemama. Safari ya kufanikisha ndoto na malengo makubwa tuliyojiwekea katika maisha yetu si rahisi rahisi kama wengi wetu tunavyodhani ama kufikiria. Kitu chochote kile chenye thamani katika maisha huwa hakipatikani kirahisi, bali juhudi, kujituma, na shauku za dhati zinahitajika.
Na kama nilivyosema awali kwamba , kuna sababu kadha wa kadha za kwa nini wengi hushindwa kufanikisha ndoto na malengo yao waliyojiwekea katika maisha. Na moja ya sababu kubwa ya hali hiyo ni kama vile nilivyosema awali kwamba , Gari lolote zuri litaharibika kama halitunzwi vizuri. Ndugu rafiki, safari ya kuelekea kufanikisha ndoto na malengo yetu makubwa tuliojiwekea katika maisha ni safari iliyojaa mabonde na milima. Ni safari iliyojaa changamoto, matatizo, na vikwazo vya kila aina. Kwa hiyo, safari yetu hii kamwe haitoweza kuja kuwa ni barabara wakati wote.
Ndugu rafiki , ili kuweza kufanikisha ndoto au malengo yoyote yale uliyojiwekea katika maisha unahitaji kuwa na nidhamu ya ustahimilivu. Katika maisha ni vizuri kuwa na malengo ila kwenye malengo hayo kama hutakuwa na nidhamu ya ustahimilivu yatakuwa ni bure kwako kwani hutafanikiwa katika jambo lolote. Kwani kwa kuwa na nidhamu kisha ukaongeza na ustahimilivu wa kuendelea kujibidiisha kwa juhudi na maarifa ni lazima utayafikia mafanikio. Ni nidhamu ya ustahimilivu pekee ndio itakayo kufanya uendelee kudumu katika kufuata malengo yako ama sivyo unaweza kutetereka na kujikuta upo mbali na malengo uliyojiwekea na kushindwa kufanikiwa. Kwa hiyo, ni muhimu sana kujenga nidhamu na tabia ya kushikamana na ndoto na malengo yako mpaka ufikie mwisho wake.
Sasa basi mara baada ya hayo naomba kwa pamoja tuweze kuangalia na kujifunza mambo manne tunayopaswa kuyadumisha ili tuweze kubakia katika mstari wa mafanikio na kuweza kufanikisha ndoto na malengo tuliyojiwekea katika maisha. Na mambo hayo manne tunayopaswa kuyadumisha ili tuweze kubakia katika mstari wa mafanikio ni kama yafuatayo:
Dumisha shauku yako;
Napoleon hill, ambaye ni mwandishi wa vitabu kadha wa kadha kama vile THINK AND GROW RICH, OUTWITTING THE DEVIL, na THE LAWS OF SUCCESS, alipata kusema kwamba ; “ The starting point of all achievement is desire”, akiwa na maana kwamba hatua ya kwanza ya mafanikio yoyote yale katika maisha ni shauku. Na akaongeza kwa kusema kwamba; shauku dhaifu huleta matokeo dhaifu kama vile moto mdogo uletavyo joto dogo. Na kwa maana hiyo ni kwamba ili kuweza kufanikiwa kaika maisha unahitaji kwanza kuwa na shauku kubwa. Ndugu rafiki, ili kubakia katika mstari wa mafanikio unahitajika sana tena sana kudumisha shauku yako. Shuku yako ndiyo itakupatia motisha na hamasa ya kuyaendea malengo yako. Na ni kweli kusema kwamba .” hakuna jambo linaloeneza shauku kama shauku” onesha shauku yako ya kudumu juu ya ndoto na malengo yako , na watu wengine watakuwa na shauku pia ya kutaka kukusaidia kufanikisha ndoto na malengo yako.
Dumisha malengo yako.
Malengo yako ndio dira yako. Malengo humsukuma mtu kufanya kazi kwa lengo la kufikia malengo aliyojiwekea. Watu wote wenye mafanikio hapa duniani wanaishi kwa malengo. Uwezo wako wa kupanga malengo ndio hatua ya kwanza katika mafanikio yako. Dumisha malengo yako. Usipoteze malengo yako kwa shughuli au kazi nyingine ambazo zitakuzuia kutumia muda, juhudi, na nguvu ambayo ndoto na malengo yako inahitaji ili iweze kufanikiwa na kukua.
Dumisha njozi yako
je , mpaka sasa bado unauona umuhimu wa ndoto na malengo yako uliyojiwekea katika maisha? Je, malengo yako bado yanaeleweka kama yalivyokuwa wakati ulipoianza safari hii ya kuelekea katika mafanikio? Je, bado unajiona ukiwa mahali fulani ndani ya miaka 2, 3, au 5 ijayo? Kama jibu ni ndiyo basi hongera sana. Na kama jibu ni hapana basi usikate tamaa, fanya hima na udumishe njozi zako. Dumisha njozi zako.
Dumisha mahusiano na mawasiliano yako
Ndugu rafiki ili kuweza kubakia katika mstari wa mafanikio katika kuelekea kufanikisha ndoto na malengo yako, basi suala la kuwa na mahusiano na mawasiliano mazuri na wengine ni suala lisilopaswa kupuuzwa. Mahusiano na mawasiliano mazuri na wengine ni mtaji muhimu sana kwako. Watu ni rasilimali muhimu sana ambayo kama itatumiwa vizuri itaweza kumnufaisha kila mmoja wetu. Kwa hiyo, jenga mahusiano na mawasiliano mazuri na wengine, kwani kwa namna moja ama nyingine watu ndio watakaoweza kukusaidia kufanikisha ndoto na malengo yako. Dumisha mahusiano na mawasiliano yako. Nakutakia utekelezaji mwema na kila la kheri.
0 Comments